Ibara 124
Utekelezaji wa maagizo ya Mahakama utafanywa nchini Tanzania kote
Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Utaratibu wa Kupeleka Hati na Kutekeleza Maagizo Yaliyomo katika Hati Zilizotolewa na Mahakama
(1)Hati zenye maagizo yaliyotolewa na Mahakama za Tanzania Bara na Mahakama za Tanzania Zanzibar katika mashauri ya madai ya aina zote na mashauri ya jinai ya aina zote (pamoja na hati za kuamuru kukamata watu) zaweza kupelekwa mahali popote nchini Tanzania na maagizo hayo yaweza kutekelezwa mahali popote nchini Tanzania kwa kufuata masharti yafuatayo:-
(a)iwapo mahakama imetoa hati zenye maagizo yatakayotekelezwa mahali ambako mahakama hiyo haina mamlaka, basi hati hiyo itapelekwa huko na maagizo yaliyomo katika hati hiyo yatatekelezwa kwa mujibu wa utaratibu unaotumika huko kwa ajili ya kupeleka hati au kutekeleza maagizo yaliyomo katika hati iliyotolewa na mahakama yenye mamlaka huko ilikopelekwa hati; na
(b)iwapo sheria inayotumika huko ilikopelekwa hati imeweka masharti kwamba hati zilizotolewa na mahakama ya mahali pengine ni lazima ithibitishwe kwanza na Mahakama yenye mamlaka mahali hapo inapotumika sheria hiyo, basi kila hati iliyotolewa na mahakama ya mahali pengine itabidi ithibitishwe kwanza kwa mujibu wa sheria hiyo kabla maagizo yaliyomo katika hati hiyo hayajatekelezwa.
(2)Iwapo mtu amekamatwa mahali popote nchini Tanzania kwa mujibu wa hati ya kuamuru kukamatwa kwake iliyotolewa na mahakama ambayo haina mamlaka mahali hapo alipokamatwa mtu huyo, basi mtu huyo atahesabiwa kuwa yuko chini ya ulinzi halali na aweza kufikishwa mbele ya mahakama iliyotoa hati hiyo,
lakini masharti haya yaliyomo katika ibara hii ndogo itabidi yatumiwe bila kuathiri masharti ya sheria inayotumika hapo mahali alipokamatwa mtu huyo.
(3)Masharti yaliyomo katika ibara hii hayatazuia sheria kuweka utaratibu kwa ajili ya kupeleka nje ya Tanzania hati zilizotolewa na Mahakama za Tanzania Bara au mahakama za Tanzania Visiwani.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.34
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.