Wakili Msomi

Ibara 53A

Kura ya kutokuwa na imani

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri na Serikali

(1)Bila ya kujali masharti ya ibara ya 51 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo na ikapitishwa kwa mujibuwa wa masharti ya ibara hii.

(2)Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, hoja yoyote ya kutaka kupitisha kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitatolewa Bungeni endapo-

(a)haina uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba hii, wala hakuna madai kwamba Waziri Mkuu amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

(b)haijapita miezi sita tangu alipoteuliwa;

(c)haijapita miezi tisa tangu hoja ya namna hiyo ilipotolewa Bungeni na Bunge likakataa kuipitisha.

(3)Hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitapitishwa na Bunge isipokuwa tu kama-

(a)taarifa ya maandishi, iliyotiwa sahihi na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia ishirini ya Wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku angalau kumi na nne kabla ya siku inapokusudiwa kuwasilishwa Bungeni;

(b)Spika atajiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuleta hoja yametimizwa.

(4)Hoja iliyotimiza masharti ya ibara hii itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

(5)Hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itapitishwa tu iwapo inaungwa mkono na Wabunge walio wengi.

(6)Endapo hoja ya kura ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu itaungwa mkono na Wabunge wengi, Spika atawasilisha azimio hilo kwa Rais, na mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku mbili tangu Bunge lilipopitisha azimio la hoja ya kura ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu atatakiwa ajiuzulu, na Rais atamteua Mbunge mwingine kuwa Waziri Mkuu.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1992 Na.20 ibara 10 Sheria ya 1995 Na.12 ibara 7

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.