Ibara 9
Ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea
Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Malengo Muhimu na Misingi ya Mwelekeo wa Shughuli za Serikali
Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, amabyo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha-
(a)kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
(b)kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;
(c)kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine;
(d)kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja;
(e)kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake;
(f)kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu;
(g)kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu;
(h)kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;
(i)kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;
(j)kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi;
(k)kwamba nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6 Sheria Na.4 ya 1992 ib.6
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.