Ibara 46
Kinga dhidi ya mashtaka na madai
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais
(1)Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, itakuwa ni marufuku kumshitaki au kuendesha mashataka ya aina yoyote juu yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.
(2)Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama raia wa kawaida ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa kwamba taarifa ya madai kwa maandishi kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na taarifa hiyo ikiwa inatoa maelezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa analodai.
(3)Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ibara ya 46A(10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9 Sheria ya 1992 Na.20 ib…
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.