Wakili Msomi

Ibara 17

Uhuru wa mtu kwenda atakako

Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu

(1)Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.

(2)Kitendochochote cha halali au sheria yoyote yenye madhumuni ya -

(a)kupunguza uhuru wa mtu kwenda atakako na kumweka chini ya ulinzi au kifungoni; au

(b)kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu kwenda anakotaka ili-

(i)kutekeleza hukumu au amri ya mahakama; au

(ii)kumlazimisha mtu kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria nyingine kuutimiza; au

(iii)kulinda manufaa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahususi au maslahi ya sehemu fulani ya umma,

kitendo hicho hakitahesabiwa au sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni haramu au ni kinyume cha ibara hii.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.