Ibara 20
Uhuru wa mtu kushirikiana na wengine
Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu
(1)Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
(2)Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) haitakuwa halali kwa chombo chochote cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na Katiba au sera yake-
(a)kinakusudia kukuza au kupigania maslahi ya-
(i)imani au kundi lolote la dini;
(ii)kundi lolote la kikabila pahala watu watokeapo, rangi au jinsia;
(iii)eneo fulani tu katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano;
(b)kinapigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano:
(c)kinakubali au kupigania matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa;
(d)kinapigania au kinakusudia kuendesha shughuli zake za kisiasa katika sehemu moja tu ya Jamhuri ya Muungano;
(e)hakiruhusu uongozi wake kuchaguliwa kwa vipindi na kwa njia za kidemokrasia.
(3)Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa na masharti ya ibara ndogo ya (2) kuhusu uhuru na haki ya watu kushirikiana na kujumuika.
(4)Bila ya kuathiri sheria za nchi zinazohusika ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote au shirika lolote, au kwa chama chochote au cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.14 ib.6
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.