Ibara 25
Wajibu wa kushiriki kazini
Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu
(1)Kazi pekee ndiyo huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu. Na kila mtu anao wajibu wa-
(a)kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali; na
(b)kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji ya binafsi na yale ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.
(2)Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), hakutakuwapo na kazi ya shuruti katika Jamhuri ya Muungano.
(3)Kwa madhumuni ya ibara hii, na katika Katiba hii kwa jumla, ifahamike kwamba kazi yoyote haitahesabiwa kuwa ni kazi ya shuruti au kazi ya kikatili au ya kutweza endapo kazi hiyo, kwa mujibu wa sheria ni-
(a)kazi inayobidi ifanywe kutokana na hukumu au amri ya mahakama;
(b)kazi inayobidi ifanywe na askari wa jeshi lolote katika kutekeleza majukumu yao;
(c)kazi ambayo mtu yeyote inabidi aifanye kutokana na kuwapo hali ya hatari au baa lolote linalotishia uhai wa ustawi wa jamii;
(d)kazi au huduma yoyote ambayo ni sehemu ya-
(i)majukumu ya kawaida ya kuhakikisha ustawi wa jamii;
(ii)ujenzi wa taifa wa lazima kwa mujibu wa sheria;
(iii)jitihada za taifa za kutumia uwezo wa kila mtu kufanya kazi kwa ajili ya kuimarisha jamii na uchumi wa taifa na kuhakikisha maendeleo na tija ya kitaifa.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.