Ibara 28
Ulinzi wa taifa
Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu
(1)Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.
(2)Bunge laweza kutunga sheria zinazofaa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa.
(3)Mtu yeyote hatakuwa na haki ya kutia sahihi kwenye mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Jamhuri ya Muungano au wa sehemu yoyote ya ardhi ya eneo la taifa na, bila ya kuathiri Katiba hii na sheria zilizowekwa, hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Jamhuri ya Muungano kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi.
(4)Uhaini kama unavyofafanuliwa na sheria utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Muungano.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.